Mbolea oza na mbolea nyingine za kikaboni zinaweza kusaidia kuongeza rutuba ya udongo na kupanua mazao. Kuna njia 2 kuu za kutengeneza mbolea oza, njia ya kurundika au kutengenezea juu ya ardhi, na njia ya shimo.
Mbolea oza huongeza virutubisho kwenye udongo, huboresha muundo wa udongo na hufanya kama mbadala wa bei nafuu kwa mbolea za kemikali ambazo pia huongeza rutuba ya udongo.
Kutengeneza mbolea oza
Ili kutengeneza mboji au mbolea oza, kwanza chimba shimo mahali penye kivuli kwenye mpaka wa shamba unapotarajia kuongeza mboji. Shimo liwe na upana wa futi nne, kina cha futi mbili na urefu wowote kulingana na nyenzo zinazopatikana.
Jaza shimo kwanza na nyenzo kama mashina ya mahindi na kisha ongeza safu ya pili yenye unene wa sentimita 15 ya mimea kavu kwa mfano nyasi kavu na majani. Nyunyiza maji juu ili kulainisha nyenzo na kuharakisha kuoza kisha ongeza safu ya tatu ya samadi ya wanyama.
Baada ya kuongeza safu ya tatu, nyunyiza na maji tena na kuongeza majivu ambayo huongeza potasiamu, fosforasi na kalsiamu, na pia hupunguza asidi zinazotokea wakati wa kuoza.
Baada ya kuongeza majivu, ongeza nyenzo zozote za kijani utakazopata kwa kina cha 15cm, kisha ongeza udongo wenye rutuba au mboji kuu. Sasa unaweza kurudia utaratibu iwapo una nyenzo nyingine, na kisha kufunika ukitumia mimea kavu.
Simika kijiti kirefu kilichochongoka kwenye rundo na ukiachie humo ili kifanye kazi kama kipimajoto. Toa kijiti mara kwa mara ili kuangalia maendeleo ya mchakato. Geuza rundo baada ya wiki mbili hadi tatu, na geuza tena wiki tatu baada ya kugeuza kwa kwanza.
Baada ya wiki sita, mbolea oza itakuwa tayari lakini ikiwa bado ina manyasi au majani basi sio tayari, na lazima ipewe muda zaidi wa kuoza.