Ufugaji wa nyuki ni mojawapo ya fursa za kibiashara zenye faida kubwa miongoni mwa wafugaji, kwani asali ni chanzo cha faida nyingi za kiafya na kimapato.
Kabla ya kuvuna asali mfugaji anatakiwa kuandaa na kupanga vifaa vya kimsingi vinavyohitajika kama vile mavazi, kofia na barakoa, glovu za mikono, gumbooti, ndoo yenye mfuniko, kitoa moshi, kisu na viberiti ili kuhakikisha usalama wakati wa kuvuna.
Shughuli za kabla ya kuvuna
Vaa nguo za kujikinga kila mara na hakikisha kwamba umelindwa vya kutosha. Jaza kitoa moshi na nyenzo za kutosha ambazo zitadumu katika kipindi cha kuvuna.
Washa kitoa moshi na uvae mavazi ya kuvunia asali.
Shughuli za kuvuna
Puliza moshi kuanzia kando mwa mzinga, chini ya mfuniko na mlangoni ili kusababisha nyuki wanaozunguka mlango kurejea ndani ya mzinga.
Kisha ondoa mfuniko na upulize moshi ili kuhakikisha nyuki walioko juu ya mzinga wanaingia ndani. Tambua pande isiyo na asali, na kwa kutumia kisu gonga mbao za juu kwani masega matupu hufanya kelele kubwa zaidi.
Tumia kisu kuondoa mbao za juu ukianzia upande usio na masega. Pulizia moshi kwa nyuki zilizo kwa masega. Ondoa nyuki kwa upole na uwaingize ndani ya mzinga. Kata masega yaliyokomaa na uyaweke ndani ya chombo.
Safisha pande za mbao za juu, zipange tena kama vile zilivyokuwa awali. Pulizia moshi kwenye juu yazo ili kuwafanya nyuki wote kuingia kwenye mzinga.
Usindikaji wa asali
Anza kwa kuvunja masega ukitumia kisu, yaweke kwenye kichungi safi, funika na kitambaa safi juu ya ndoo.
Funika chombo na mfuniko ili hewa isiingie. Hifadhi asali iliyochujwa kwenye vyombo vya plastiki.