Wakulima mara nyingi hutumia pesa nyingi kununua mbolea za kemikali na viuatilifu. Ingawa hii inaweza kutoa mavuno makubwa kwa muda mfupi, kutumia kemikali hizi kwa muda mrefu kunaweza kuathiri udongo, mazingira na watu kwa kuua viumbe hai vilivyo kwenye udongo.
Afya ya udongo ni muhimu kwa mimea na vijidudu. Vijidudu ni muhimu katika kudumisha mimea pamoja na kurutubisha udongo, hivyo kulinda mimea dhidi ya magonjwa.
Aina mbalimbali za michanganyiko zinaweza kutayarishwa ili kusaidia vijidudu vyenye faida kukua vyema kwenye udongo. michanganyiko hii ni ya kikaboni na hutengenezwa kutoka kwa nyenzo asili kwa gharama nafuu.
Vijidudu hurutubisha udongo, na pia huongeza mavuno.
Maandalizi ya mchanganyiko wa kikaboni
Viambato vinavyohitajika ni: Kilo 1 ya unga ulio na protini nyingi kama vile unga wa kunde, kiganja cha sukari, kilo 1 ya kinyesi kibichi cha ng’ombe, kilo 1 ya majani ya mwarobaini, lita 1 ya mkojo wa ng’ombe na lita 10 za maji.
Changanya viambato hivi vyote kwenye ndoo. Changanya kinyesi cha ngombe na maji, na uviongeze kwenye ndoo pamoja na viambato vingine ili kutengeneza mchanganyiko. Ongeza maji na koroga mchanganyiko ukitumia kijiti cha mbao mara mbili kwa siku kwa dakika tano, kisha funika ndoo.
Mchanganyiko huo huwa tayari baada ya siku 10 kwani vijidudu huwa vimekua na vimeongezeka idadi. Unaweza kujua kwamba mchanganyiko uko tayari kwa harufu yake.
Viambato na matumizi
Majani ya mwarobaini yanayotumika husaidia kudhibiti wadudu waharibifu kama vile vidukari kwenye mimea. Unga ulio na protini nyingi hulisha vijidudu. Mkojo wa ng‘ombe hutoa naitrojeni ambayo hudumisha vijidudu. Maji hutoa nafasi ambamo vijidudu huishi na kuzaliana. Kinyesi cha ng‘ombe kina vijidudu vingi.
Kwa matumizi, weka mchanganyiko kwa mbegu ili kuzitibu na zikaushie kwenye kivuli. Mchanganyiko unaweza kutumika kenye mizizi ya miche ili kuhimiza ukuaji.
Ili kunyunyizia mimea, yeyusha lita 1 ya mchanganyiko kwenye lita 100 za maji mara moja kwa wiki au mara moja kwa wiki mbili wakati mimea inakua, inachanua maua au inapotoa matunda. Mchanganyiko huo unaweza kutumika kurutubisha udongo.