Kuunganisha au kubebesha ni mbinu ambayo hutekelezwa sana na wakulima wengi, pamoja na watunza bustani ulimwenguni kote ili kuunda mimea ya kipekee.
Sehemu ya juu ya mmea uliounganishwa huitwa kikonyo na sehemu ya chini huitwa mche shina. Kuunganisha mimea kuna manufaa makubwa zaidi hasa kwa wakulima wa matunda. Kuna njia mbalimbali za kuunganisha ambazo ni rahisi kujifunza.
Faida za kuunganisha kwa wakulima
kuunganisha hutengeneza aina za mimea ya kipekee hasa matunda ambayo yanaovutia kwa wakulima na wateja, na hivyo kuongeza soko.
Kwa kuwa baadhi ya miti hushambuliwa na magonjwa wakati wa hali mbaya ya hewa, hivyo kuunganisha huongeza ustahimilivu dhidi ya magonjwa haya. Mimea iliyounganishwa hutoa matunda na maua mapema ikilinganishwa na ile ambayo haijaunganishwa.
Vifaa vinavyotumika kuunganisha miche ni gharama nafuu vikilinganishwa na kupanda mimea kutoka na mbegu, na hivyo kuwaepusha wakulima kutumia fedha nyingi.
Kuunganisha vile vile husababisha matunda bora, majani bora, na maua bora kulinganishwa na mimea inayokuzwa kutoka kwa mbegu. Kuunganisha pia husaidia kubadilisha umbo la mmea kutoka jinsi ilivyokusudiwa kuwa awali.