Kilimo mseto ni mchanganyiko wa kilimo na misitu.
Uhusiano ulio kati ya miti na mazao huongeza manufaa ya kijamii, kiuchumi na kimazingira. Kuna ainisho kuu tatu za kilimo mseto yaani; mfumo wa silvoarable ambao ni mchanganyiko wa miti na mazao, mfumo wa silvopastoral ambao hujumuisha miti na wanyama, na mfumo wa agrosilvopastoral ambao hujumuisha mchanganyiko wa miti, wanyama na mazao.
Umuhimu wa miti
Katika kilimo cha kawaida, ukataji miti ovyo ni jambo la kawaida lakini miti ina mihimu kadhaa kwa mazao na wanyama. Mizizi ya miti inapozidi kwenda chini kuliko ile ya mazao, maji yanaweza kupenyeza ardhini kwa urahisi zaidi , jambo ambalo hupunguza utuamaji wa maji na pia hupunguza mtiririko kasi wa maji, na hivyo hudhibiti mmomonyoko wa ardhi.
Miti pia huchukua madini kutoka kwenye tabaka za udongo zenye kina kirefu, ambazo haziwezi kufikiwa na mazao. Hii huzuia uvujaji wa madini na virutubisho kwenye maji ya chini.
Matawi ya miti hufanya kama vizuizi vya upepo mkali, jambo ambalo hupunguza uvukizaji wa maji kutoka kwenye mimea. Miti pia hufanya kama makazi ya wanyamapori, na huongeza ustawi wa wanyama.
Ushirikishwaji wa miti katika kilimo huongeza idadi ya viumbehai, na husaidia katika udhibiti wa wadudu kibayolojia kwa kuvutia ndege ambao hula viwavi kwa mfano.
Miti inaweza kupanua njia za kipato cha mkulima. Huku kunaweza kufanya kwa kutolea mifugo malisho, na kutoa chakula kama vile matunda na karanga, pamoja na kuni na mbao.