Kutengeneza mbolea ya minyoo hutekelezwa kwa kutumia minyoo kuozesha taka.
Kuna aina nyingi za minyoo kulingana na jinsi wanavyoozesha taka. Minyoo bora zaidi huitwa minyoo myekundu. Minyoo myekundu hula taka nyingi kwa siku, wanaweza kutengeneza mboji mara moja na idadi yao huzidisha haraka sana. Mnyoo aliyekomaa hutaga yai kila mwezi, ambayo huanguliwa kwa mwezi na kutoa minyoo 3–5. Ufugaji wa minyoo huenda sambamba na kilimo hai na wakulima wanaweza kupanda mazao ya kilimo hai kupitia mboji hii.
Umuhimu wa minyoo
Minyoo hula taka kama vile taka za jikoni, magugu na samadi. Takataka kutoka sokoni zinaweza kubadilishwa kuwa mboji kwa kutumia minyoo, na hivyo kupunguza uchafuzi wa mazingira. Minyoo wanaweza pia kuzalishwa na kuuzwa kwa wakulima wengine.
Mazao ya kilimo-hai yanayolimwa kupitia mboji ya minyoo ni bora, na huuzwa bei nzuri sokoni. Soko la minyoo halina kikomo kwani wanaweza kuuzwa ndani ya nchi au kusafirishwa nje unahitaji tu uthibitisho ili kuuza nje.
Viwango vya kilimo cha mbolea minyoo
Kiwango cha chini kabisa ni kununua kilo 1 ya minyoo, na kuweka taka za jikoni kwenye dumu la lita 20 na kuongeza minyoo. Hii itatumika kwa bustani ndogo ya jikoni. Utaweza kupata mboji ya minyoo na mbolea ya maji ya minyoo kutoka humo. Kwa bustani kubwa, tumia pipa za plastiki na angalau kilo 2–5 za minyoo.
Kipindi cha kutengeneza mboji kinaweza kuchukua hadi miezi 3 ikiwa umetumia kilo 5, na huchukua muda mrefu ikiwa utatumia chini ya kilo 5, ambacho ni kiwango cha pili. Kwa kiwango cha tatu, unaweza kutumia vitanda vya saruji au mbao.