Kilimo cha hydroponic kinahusisha upandaji wa mimea bila kutumia udongo. Aina hii ya kilimo haihusishi mbinu nyingi, na inaweza kupokelewa kwa urahisi na wakulima.
Kuna nyenzo za msingi zinazohitajika ambazo ni pamoja na mbegu safi, maji safi na trei ya alumini ili kuzuia kutu. Mbegu za shayiri huanza kuota baada ya siku moja. Hata hivyo, wakati wa kuvuna shayiri zingatia aina ya mnyama utakaomlisha. kwa mfano, kwa nguruwe na sungura vuna shayiri katika siku 6 na kwa ng‘ombe, mbuzi na kondoo vuna katika siku 8.
Hatua za kupanda
Kwanza pima uzito wa mbegu ambazo zinaweza kutoshea kwenye trei na uziloweke ndani ya maji kwa muda usiozidi saa 4.
Kisha ondoa maji na ufunike mbegu ndani ya ndoo iliyo na matundu juu ya mfuniko ili kuwezesha uingizaji mzuri wa hewa ya oksijeni, na hivyo kuhimiza uota.
Mwaga kiganja cha maji kwenye mbugu kila baada ya saa 12 ili kudumisha unyevu, tikisa mbegu ili zichanganyike vizuri. Kisha panda mbegu kwenye trei safi na uzitandaze kwa usawa ukitumia mkono ili kuhimiza uotaji sawa.
Hakikisha umeacha nafasi ndogo kwenye ncha moja ya trei ili kuepusha mizizi ya malisho kuziba matundu ya trei. Weka trei kwenye eneo la kukuzia malisho, huku upande wenye matundu ukielekea chini.
Mwagilia mbegu za shayiri angalau mara 3 kwa siku, na vuna kulingana na aina ya mnyama utakaomlisha.