Nyanya huathiriwa na idadi ya magonjwa. Bakajani tangulia na madoa ya majani ndio magonjwa ya kawaida zaidi, na yanahitaji kuzingatiwa.
Bakajani tangulia na madoa ya majani hushambulia mmea kuanzia chini na huendelea juu hadi mmea mzima uathirike. Magonjwa haya husababisha madoa kwenye majani na majani kugeuka manjano, kisha hudhurungi na hatimaye kuanguka. Hii huathiri mmea wote iwapo haijatibiwa. Hata hivyo magonjwa haya hayathiri matunda moja kwa moja kama vile chule.
Kutambua ugonjwa
Madoa ya majani huonekana kama madoa madogo kwenye majani. Bakajani tangulia huonekana kama madoa makubwa.
Mvua kubwa, unyevu mwingi, umande wa asubuhi, msongamano mkubwa wa mimea na maeneo ambayo hayajatandazwa, huhimiza ukuaji wa magonjwa na matukio ya bakajani na madoa ya majani huwa mengi.
Kuzuia na Kudhibiti
Kuweka matandazo, kuacha nafasi ifaayo na kunyunyizia viuakuvu husaidia kuzuia bakajani na madoa ya majani. Lakini mimea ikishambuliwa na ugonjwa huo, tunaweza tu kuzuia kuenea zaidi kwa kutumia viuakuvu kila baada ya siku 7 hadi 10.