Sungura huzaa sana, sungura jike anaweza kuzaa watoto 30 kwa mwaka. Nyama ya sungura ni tamu, ina protini nyingi na mafuta kidogo. Wafugaji wengi huwafuga sungura kwa sababu wanahitaji wakati kidogo na nafasi ndogo na hivyo, huwawezesha kupata pesa zaidi haraka.
Kuwawezesha sungura kukua vizuri na kuzaa haraka, ni muhimu kuwalisha vyema. Wakiwa wamefugwa, sungura hula: Mimea mbichi kama vile tridax daisy, makuti ya mnazi na majani ya njugu zilizovunwa hivi juzi. Mizizi na majani ya karoti yanafaa kulishwa sungura kwa kiwango cha kutosha.
Kuzuia magonjwa
Yakaushe majani au nyasi kabla ya kuwapa sungura ili kuwalinda dhidi ya kuhara na uvimbe unaosababishwa na vimelea vilivyo kwenye majani ambayo yana umande. Baadhi ya majani mabichi kama vile majani ya mpera na mbaazi husaidia kutibu kuhara. Majani ya mwarobaini na mtukutu husaidia kuzuia ugonjwa wa kuhara damu. Katika msimu wa kiangazi, majani ya njugu na maharagwe yaliyoachwa baada ya kuvuna yanaweza kutumika na kuhifadhiwa nyumbani mahali pakavu.
Hatari ya kupata upele
Sungura waliyo na utapi ya mulo hushambuliwa sana na upele. Sungura aliye na upele ana vidonda mwilini, miguuni na masikioni na ni dhaifu. Wakiwa na upele sungura hawali vizuri, hivyo wanakua polepole na huzaa watoto wachache. Kwa hivyo, changanya majani na chakula cha kununuliwa ambacho kitawapa sungura nguvu, madini, protini na vitamini.
Tengeneza chakula kama cha kununuliwa kwa kuchanganya mahindi, wishwa wa ngano, soya yaliyokaangwa, maganda ya chaza, mizizi ya mihogo na chumvi. Majani ya moringa husaidia katika ukuaji wa sungura na kuua viini.
Kiasi cha chakula
Wape sungura jike waliyo na watoto 250g hadi 300g, na umpe sungura jike aliye na mimba 120g. Mpe sungura dume anayezalisha 100g, na kati ya 20g hadi 100g kwa sungura mchanga kutegemea umri wake.
Chagua muda maalum wa kulisha sungura kila siku ili kupunguza mafadhaiko kwa mnyama. Sungura wanafaa kuwa na maji safi kila wakati.
Vyombo vya kulishia vinafaa kuwa vizito na kutundikwa kwenye banda ili sungura wasikanyage ndani na kuwaga maji. Ukiwa na vyombo vyenye mashimo, sungura wachanga wanaweza kula kupitia mashimo yaliyo chini na, mama sungura hula kupitia shimo la juu, na hivyo hawawezi kumwaga chakula.