Kuwa ni mnyama muhimu kwa lishe na utoaji wa malighafi kwa viwanda, ubora na wingi wa nguruwe huamuliwa na teknolojia zinazotumiwa katika uzalishaji wake.
Usimamizi wa nguruwe unajumuisha na utekelezaji wa mbinu bora za uzalishaji ambazo ni pamoja na mbinu za usimamizi wa makazi, mbinu za ulishaji, mbinu za kuzaliana, na mbinu za utunzaji wa afya ya wanyama ili kupata matokeo bora katika mradi.
Mbinu za usimamizi
Kwa makazi, nguruwa wanaweza kufugwa nje au ndani ya mabanda. Hata hivyo, mfumo wa kufugia nguruwe nje haupendelewi kwani wanaweza kupata magonjwa kwa urahisi. Mfumo wa kufugia nguruwe ndani ya banda ni bora. Mfumo wa kufugia nguruwe ndani unahusisha ujenzi wa mabanda bora katika mahali pazuri palipo uingizaji mzuri wa hewa na mwanga wa jua. Sakafu ya zege isiyoteleza inapaswa kujengwa kwa usafishaji rahisi. Paa lazima lisipitishe maji, na vizuizi viwekwe zizini ili kuzuia vifo vya nguruwe wachanga vinavyosababishwa na kukanyagwa na nguruwe mama.
Vile vile, vyombo vya kulishia na kunyweshea vinapaswa kuwekwa katika kila chumba cha nguruwe, na lazima ukuta uwekwe ili kugawanya kati ya kihori cha maji na kihori cha chakula. Chakula kinachotolewa kinapaswa kuwa na uwiano wa wanga, protini, vitamini na madini. Chakula kinapaswa kuwa na zaidi ya 70% ya wanga inayopatikana kutoka kwa vyanzo kama vile nafaka na punje. Mahitaji ya protini hutofautiana kulingana na aina ya nguruwe, na vyanzo vyake ni pamoja na unga wa mbegu za mafuta, unga wa samaki na unga wa nyama. Madini yanayohitajika ni kalsium, fosforasi, chuma, manganis, zinki na ayodini kwa uyeyushaji mzuri wa chakula na kuimarisha mafupa ya wanyama.
Nguruwe jike bora anaweza kuzaa hadi watoto 15 mara moja. Uhamilishaji asilia na bandia hutumika kwa ajili ya kuzaliana. Hata hivyo, uhamilishaji bandia hupunguza majeraha. Wakati mzuri wa uhamilishaji bandia ni saa 15–24 baada ya jike kuwa kwenye joto.
Kabla ya kuzaa, tenganisha nguruwe mjamzito na mweke kwenye zizi la kuzalishia na mpe chakula bora saa 12 kabla ya kuzaa. Mchakato wa kuzaa huchukua masaa 1–6. Wape nguruwe wachanga maziwa saa moja baada ya kuzaliwa, na waweke kwenye sunduku kavu na safi yenye matandiko safi, na joto. Safisha matiti vizuri kila wakati wa kulisha, na walishe watoto kila baada ya muda wa masaa 1–2. Walishe chakula cha madini ya chuma ili kuzuia upungufu wa damu. Unaweza pia kuwalisha watoto kwa mikono iwapo nguruwe mama amekufa. Tenganisha watoto na mama miezi 2 baada ya kuzaliwa. Wape watoto dawa ya kuua minyoo mara moja kila baada ya miezi 3, na wachanje dhidi ya magonjwa kama vile homa katika umri wa miezi 2. Nguruwe wachanga walioathiriwa na minyoo hupatwa na ugonjwa wa kuhara, kupungua uzito, matatizo mapafuni na mwishowe kifo. Upungufu wa lishe na madini husababisha uharibifu wa ngozi na manyoya, upooza, upofu na kifo. Magonjwa ya nguruwe ni pamoja na homa, mapafu, kimeta, na ugonjwa wa mguu na mdomo, erisipela na upungufu wa damu.