Nzi wa matunda hutaga mayai yao kwenye matunda na matunda huanza kuoza. Hii husababisha hasara kubwa haswa kwa soko la kuuza nje. Hasara hizi zinaweza kudhibitiwa kwa kutumia mitego ya pheromone za methyl eugenol.
Mitego hutengenezwa kutoka kwa mikebe ya plastiki kwa kutoboa mashimo madogo juu ya kila pande ya mkebe. Pia, toboa mashimo chini ya mkebe ili kuzuia maji ya mvua kuingia ndani ya mkebe.
Weka kamba kupitia kifuniko na kuninginiza mtego chini ya kivuli cha mti kwa urefu unaoweza kuona kwa urahisi. Kwa upande wa ndani funga kidonge cha pheromone kikishikiliwa kwa kamba. Badilisha vidonge vya pheromone (kemikali za hisia za wadudu) baada ya miezi 6.
Ninginiza kati ya mitego 10-40 kwa kila hekta. Weka mitego karibu na maeneo ya kutupa taka, na katika mipaka ya shamba. Unaweza pia kunyunyiza chambo cha chakula kilichochanganywa na viuatilifu kwenye ukingo wa shamba mara moja kwa wiki.
Kuunda mitego ukitumia chupa za plastiki
Mitego pia inaweza kuundwa kwa kutumia chupa za maji za plastiki. Toboa mashimo 2 ya 3cm kwa upana katika sehemu ya juu ya chupa. Kisha toboa shimo kwenye kifuniko ili upitishe waya.
Tengeneza utambi wa pamba ili ushikilie pheromone (kemikali za hisia za wadudu) iliyochanganywa na dawa ya kuua wadudu. Lakini tumia dawa ya kuua wadudu isiyo na harufu. Changanya ujazo unne (4) wa pheromone na ujazo moja wa dawa ya kuua wadudu.
Weka kifundo cha pamba kwenye waya, na uweke utambi kwenye chupa . Ninginiza mtego kwenye tawi la mti. Unaweza kutumia mtego mmoja kwa kila mti mwezi mmoja baada ya maua kuchana hadi wakati wa kuvuna matunda.
Harufu hupungua baada ya muda. Kwa hivyo ni sharti ibadilishwe kila baada ya mwezi. Kwa kilimo hai cha matunda, usitumie dawa ya kuua wadudu lakini tumia mitego maalum ambayo hairuhusu nzi wa matunda kutoroka baada ya kuingia.