Ni tamanio la kila mfugaji wa kuku kuwa na kuku ambao hukua haraka. Ikiwa hili halitafanikiwa, mfugaji wa kuku hupata hasara.
Ukuaji wa polepole unaweza kusababishwa na maumbile duni ya kuku. Hili linaweza kutokea wakati wa ukuaji wa kiinitete cha yai ambacho kinaweza kudhoofisha ukuaji wa haraka. Hali hii haiwezi kutibika, hivyo basi hakikisha kwamba unapata vifaranga kutoka kwenye sehemu inayoaminika.
Mambo mengine ambayo huzuia ukuaji wa haraka
Msongamano mkubwa. Hii huweka kifaranga kwenye hali ya kujidonoa, na husababisha magonjwa mengi ambayo huathiri ukuaji wa ndege. Kwa mfano, msongamano mkubwa unaweza kusababisha ndege kujila wenyewe, jambo ambalo husababisha ndege dhaifu kutokula na hivyo ukuaji wao huathiriwa. Hili linaweza kudhibitiwa kwa kutoa uingizaji mzuri wa hewa, kutoa vihuri vya maji na chakula vya kutocha.
Mbinu duni za kushughulikia vifaranga. Siku 7 za kwanza wakati wa kushughulikia vifaranga ni muhimu sana katika maisha ya vifaranga. Tumia siku hizi za kwanza kuboresha ukuaji wa vifaranga kwa sababu kosa lolote linalofanywa katika suala la malisho, chanjo, hali ya joto halitaathiri ukuaji wa vifaranga tu bali pia maisha yao yote.
Ukosefu wa vihori vya malisho na maji vya kutosha. Ili kupunguza idadi ya kuku wa ukubwa mdogo, toa vihori vya malisho na maji vya kutosha. Vihori vya malisho vinapaswa kuwa karibu na vihori vya maji.
Ukosefu wa lishe bora. Malisho yaliyoandaliwa na viungo duni hutoa matokeo duni.
Uwepo wa vimelea. Hivi vinaweza kuwa vya ndani au vya nje. Vimelea husababisha mafadhaiko kwa kuku, jambo ambalo hupunguza ukuaji wa ndege.
Ugonjwa. Uwepo wa ugonjwa katika kundi la kuku utasababisha ukuaji duni kwa sababu ndege wagonjwa hawali na kunywa. Chanja ndege ili kudhibiti magonjwa makubwa kama vile kideri.