Chakula cha kuku huchangia asilimia 70% ya gharama za uzalishaji wa kuku. Kutengeneza malisho yako nyumbani husaidia kupunguza gharama na kuongeza kipato.
Ni muhimu kuwalisha ndege vyakula bora vyenye lishe kwa ukuaji sahihi, uzalishaji wa mayai na afya bora. Pia ni muhimu kuongeza protini kwenye chakula ili kusaidia vifaranga kukua haraka. Chakula cha kuku kilichochachushwa hupendekezwa kwa kuwa ni rahisi kumeng’enywa. Hata hivyo, wape kuku mboga za majani. Epuka kutumia nyenzo zilizooza kutengeneza malisho kwa sababu zinaweza kuwa na sumu ambayo ni hatari kwa ndege.
Mbinu ya chakula cha kuku
Mbinu hii inahusisha kuchanganya mahindi kilo 20, alizeti kilo 12, mtama/ngano kilo 13, soya kilo 5, chumvi gramu 200 ili kukidhi mahitaji ya lishe ya kuku.
Haya yanapaswa kusagwa au kuchachushwa kwa siku 3 ili kurahisisha ulaji wa chakula.
Mbinu ya Premix
Mbinu hii inapendekezwa kwa aina zote za ndege. Inahusisha kuchanganya chakula cha mkusanyiko na mahindi yaliyosagwa katika uwiano wa kopo 3 za mahindi kwa kopo 2 chakula cha mkusanyiko. Viungo hivi vinapaswa kuchanganywa vizuri ili kuwawezesha ndege kupokea viungo sawasawa.
Chakula cha kuku kilichosagwa
Hii ndiyo mbinu ya bei nafuu zaidi ya kutengeneza vyakula vya kuku. Hata hivyo chakula hiki hakifai kwa kuku wa nyama na kuku wa mayai, bali kwa kuku wanaofugwa kwa njia huria. Mbinu hii inahusisha kuchanganya ushwa wa mahindi, ngano na alizeti kwa uwiano wa 3:2:1. Pia unapolisha, mpe kila kuku kilo 0.13 kwa siku. Mwishowe, hakikisha kwamba chakula cha kuku kimehifadhiwa mahali pakavu, penye baridi, na kagua chakula ili kuchunguza wadudu kabla ya kuwalisha ndege.