Mbinu ya kupanda mazao bila udongo inachukuliwa kuwa njia mpya ya kilimo duniani kote, na njia hii inajulikana kama haidroponiki. Mbinu hii imekuwepo kwa maelfu ya miaka kuanzia 1600BC.
Katika karne ya 21, kilimo cha haidroponiki kimekuwa njia ya wakaazi wa mijini ulimwenguni kote, na pia nchini Kenya.
Faida za haidroponiki
Faida ni, matumizi ya nafasi ndogo, ni kilimo cha busara na usafi kwani hutumii udongo. Kwa hivyo, huwezi kupata uchafu wakati wa kilimo hiki, kilimo hiki huokoa hadi 80% ya maji, mimea hukua haraka kwa sababu ya virutubisho vinavyotolewa.
Pia kuna wadudu na magonjwa maachache tu kwa sababu ya kupunguza matumizi ya udongo. Hata hivyo, unashauriwa kutumia viuatilifu ambavyo havina madhara magonjwa yakitokea.
Aina za vitengo vya haidroponiki
Kuna vitengo viwili tofauti, kitengo cha mazao na kitengo cha mifugo. Kuna mifumo mbalimbali ambayo mkulima anaweza kufuata. Kitengo cha kwanza cha mfumo ni mbinu ya utando wa virutubishi (NFT); na hii hujiendesha kwani inahitaji pampu ya kusukuma maji kutoka kwenye tanki hadi kwenye mazao na inaweza kustahimilia mimea 450.
Sehemu ya pili ya mfumo ni bustani ya jikoni; na inafaa kwa mtu yeyote ambaye anataka kutumia nafashi yake ndogo nyumbani. Katika mfumo huu mazao humwagiliwa maji kwa mikono, na unaweza kushikilia mazao 300.
Kutekeleza vitengo
Mfumo wa NFT hutumia mabomba madogo meusi kumwagilia maji kwa mazao kupitia vikombe vya plastiki. Wakati wa kumwagilia, virutubishi vya haidroponiki huwekwa ndani ya maji na na husukumwa hadi kwenye mmea wa mwisho na maji. Mbinu hii ni nzuri kwa ukuaji wa letasi, brokoli, koliflawa, mchicha na sukumawiki.
Kwa bustani ya jikoni, umwagiliaji wa maji hufanywa kwa mikono. Bustani ni nzuri kwa upandaji wa zabibu, mchicha na korongo na inaweza kushikilia mazao 300.