Katika nchi nyingi, ukuzaji wa mazao hufanywa katika msimu wa mvua ingawa baadhi ya wakulima hupata maji ya kukuza mimea ya mboga ya bei ya juu wakati wa kiangazi.
Kutonesha maji huokoa wakati, hupunguza kazi, udongo haujifungi haraka na pia humwaga maji pole pole na kwa usawa. Kutonesha maji pia huruhusu mimea kukua vyema na kutoa mavuno mengi, pamoja na kuokoa maji na kuzuia kuenea kwa magonjwa.
Jinsi ya kuanzisha utaratibu wa kutonesha maji.
Awali, andaa vitalu vilivyo na urefu wa 15m kwa upana 1.6m. Lainisha udongo, na uongeze mbolea oza. Kisha, sawazisha vitalu.
Toboa shimo ndogo chini ya chombo cha plastiki na uweke kitambaa ili kuchuja maji yanayotoka kwa hifadhi (chombo) kuingia katika mrija. Hakikisha chombo kinakaa thabiti ili kustahimili maji. Chombo kinafaa kuwa kimesawazishwa, na kuinuliwa juu urefu wa 90cm.
Weka mirija 2 ya 15m, kila mmoja ukiwa umbali wa 60cm. Toboa mashimo madogo kwa mirija yakiangalia juu ili kuzuia udongo kuyaziba.
Baada ya kuezeka mfumo na kujaza hifadhi cha maji, panda miche asubuhi wakati udongo una unyevu wa kutosha. Panda miche kwa pande zote mbili za mrija kwa kila shimo, ukiacha umbali wa 30cm kati ya miche. Funika miche ukiweka matandazo ili kuhifadhi unyevu udongoni.
Baada ya kupandikiza miche, jaza chombo cha maji mara moja kila siku. Bomba la injini au la kusukuma hupunguza kazi ya kujaza chombo cha maji. Punguza kumwagilia maji mara tu matunda yatakapokomaa ili kuharakisha kuiva.
Linda na kutengeneza mfumo wa kutonesha kwa kusafisha chombo cha maji kila wiki au wakati wowote inapohitajika ili kuondoa uchafu ambao unaweza kuziba mrija.