Nyuki wana faida nyingi kwa mwanadamu, ambazo ni pamoja na kutoa asali.
Kabla ya kuondoka kwenda kuvuna asali, mfugaji wa nyuki lazima aandaliwe na vifaa ambavyo ni pamoja na; vazi la kuvunia, kofia na barakoa, glavu, viato, ndoo safi yenye mfuniko, kitoa moshi, kisu na kiberiti. Ili kufanikiwa na uvunaji wa asali, vaa nguo zako za kujikinga na uhakikishe kuwa umelindwa vya kutosha.
Kukusanya masega ya asali
Jaza kitoa moshi na nyenzo za kutosha ambazo zitadumu katika kipindi chote cha uvunaji. Wakati wa kuvuna, pulizia moshi kuzunguka mzinga na mlangoni mwa mzinga ili kusababisha nyuki kuingia ndani mwa mzinga.
Subiri kidogo na kisha ondoa mfuniko wa mzinga na upulize moshi ili kuhakikisha nyuki walioko juu ya mzinga wanaingia ndani.
Tambua upande usio na asali, na kwa kutumia kisu gonga mbao za juu kwani masega matupu hufanya kelele kubwa zaidi. Kata masega yaliyokomaa na uyaweke ndani ya chombo
cha plastiki ukianza na upande usio na asali.
Safisha upande wa mbao za juu na uzipange upya kama vile zilivyokuwa awali. Anza kwa kuvunja masega ukitumia kisu, yaweke kwenye kichungi safi, funika na kitambaa safi juu ya ndoo.
Usindikaji wa asali
Ndoo safi na kichungi vinahitajika katika usindikaji wa asali. Kata masega katika vipande vidogo na uyaweke kwenye kichungi safi , n ufunike na kitambaa safi juu ya ndoo.
Funika chombo na mfuniko ili hewa isiingie. Hifadhi asali iliyochujwa kwenye vyombo vya plastiki.