Ili kufanikiwa na kilimo cha kahawa, kuna mbinu mbalimbali ambazo husaidia kuongeza tija.
Kahawa hustawi vyema katika maeneo yenye mzunguko mzuri wa hewa na udongo wenye rutuba. Ili kupanda kahawa, chimba mashimo ya futi 2 za mraba kwa kina cha futi 2 , huku ukitenganisha udongo wa juu na udongo chini. Ikiwa una mbolea oza au samadi ya maji, ichanganye na udongo wa juu ili kuongeza rutuba na mboji. Jaza shimo kwa udongo wa juu, kisha weka kijiti katikati ya shimo na uliache kwa muda wa mwezi mmoja. Shimo lililotengenezwa vizuri ni muhimu kwa tija bora.
Kupanda na kusimamia kahawa
Baada ya kutengeneza shimo, chimba tundu dogo katikati mwa shimo kwa kutumia kiganja au jembe dogo na upanda mche. Ongeza udongo kuzunguka mmea ili maji yasituame karibu na shina.
Palilia kuzunguka mmea ili kuhifadhi unyevu. Acha nafasi kati ya mmea na matandazo na weka majivu kwenye nafasi hiyo ili kudhibiti wadudu.
Baada ya miezi 9 hadi 10, kunja shina la kahawa ili kutoa matawi mengi. Ili kutekeleza hatua hii, kunja shina la kahawa kuelekea ardhi kwa upole kwa pembe ya digrii 45. Simika kijiti ardhini na ufunge shina la kahawa kwenye kijiti hicho.
Baada ya muda wakati tija ya kahawa imepungua, kata mashina yote ya kahawa na uache tu shina moja changa. Baadaye, kata machipukizi mengine na uache takriban machipukizi 4 yenye afya.