Muhogo huchukua takribani mwaka mmoja kukomaa na kuvunwa. Kupanda mseto wa zao la muhogo na mazao mengine, kwa mfano mahindi humwezesha mkulima kupata mapato baada ya miezi mitatu.
Muhogo unaweza kulimwa mseto na mazao mengi ambayo ni pamoja na mikunde kama vile maharagwe, soya, mbaazi, karanga, nafaka kama vile mahindi, na mazao mengine ya mizizi kwa mfano viazi vitamu. Kupanda mseto wa mahindi na muhogo hupunguza mavuno ya muhogo, lakini mseto mzuri unahakikisha kuwa unapunguza changamoto hiyo kwa vile mapato yatokanayo na zao la mseto ni makubwa kuliko mapato ya muhogo pekee.
Mambo ya kuzingatia ili kupanda mseto
Ili kupanda mseto wa mahindi na muhogo, chagua aina bora za mihogo na mahindi. Mihogo inapaswa kusimama wima na kutoa matawi ya wastani, huku mahindi yawe aina ya muda mfupi wa ukomaavu kama siku 90.
Weka mbolea kwenye udongo wenye rutuba ya wastani. Ikiwa rutuba ya udongo ni duni sana, weka mbolea ya kikaboni kabla ya kuongeza mbolea ya madini. Viwango vya mbolea vinavyopendekezwa ni gunia sita za 50kg NPK kwa kila hektari wakati wa kupanda. Ongeza mfuko mmoja wa urea ulio na kilo 50 wiki 3 baada ya kupanda. Pia ongeza mfuko mmoja wa kilo 50 za urea wiki 5 baada ya kupanda. Weka mbolea iwapo mapato ya ziada kutokana na ongezeko la mavuno ni makubwa kuliko gharama ya mbolea.
Kupanda, na kuweka mbolea
Ukipanda mihogo kwenye matuta, tenganisha matuta kwa umbali wa 1m. Panda mihogo na mahindi kwa wakati mmoja, huku mashina ya muhogo yakisimishwa au yakiinamishwa. Mahindi hupandwa kwa umbali wa sm 15 kutoka kwa muhogo iwapo matuta yametengenezwa. Iwapo matutu hayajatengenezwa, panda mahindi katikati ya safu za mihogo.
Weka mbolea ya NPK kwenye shimo la kina cha sentimita 5 karibu na mahindi baada ya kupanda 5cm mbali na mahindi. Wiki 3 baada ya kupanda, tengeneza mashimo madogo ya kina kifupi kwa umbali wa sm 20 kutoka kwenye mahindi na uweke mbolea ya urea kwenye mashimo hayo. Kisha weka mfuko mwingine wa urea baada ya wiki 5.
Ikiwa udongo una rutuba sana au unapanga kuweka mbolea, panda mahindi kwenye msongamano mkubwa wa 25cm kati ya mimea, lakini iwapo udongo una rutuba ya wastani, panda kati ya safu kwa umbali wa 50cm.