Mahindi ni zao la nafaka muhimu linalolimwa ulimwenguni kote. Mahindi ni chanzo kizuri cha kabohaidreti, protini, vitamini, na madini. Mahindi yanaweza kutumiwa kama uji, ugali, na pombe.
Pia hutumika moja kwa moja kama chakula cha mifugo. Kupanda mahindi ni rahisi kwa vile kunahitaji mtaji mdogo, hukomaa haraka (miezi 2 hadi 5), rahisi kulima na soko lake linapatikana kwa urahisi. Mahindi pia hayastawi katika kivuli kwa vile yanahitaji jua zaidi. Panda aina zilizoboreshwa kutoka kwa vyanzo vinavyoaminika ili kupata mavuno mengi kwani aina hizi ni sugu dhidi ya wadudu na magonjwa.
Kilimo sahihi cha mahindi
Chagua udongo usio na maji mengi sana, na wenye rutuba, na udongo wa kichanga ulio tifutifu, ambao una mboji. Safisha shamba kwa kuondoa magugu na vitu vingine visivyohitajika, pamoja na kutengeneza matuta, na kutunza rutuba ya udongo.
Panda mapema ili kuruhusu mimea kukua kabla magugu hayajaibuka. Hakikisha unapanda mseto wa mahindi na mimea isiyoshindania virutubisho na maji ili kuvunja mzunguko wa maisha ya ugonjwa.
Panda mbegu 3 kwa kila shimo, kwa muachano wa sm 75 kati ya safu na sm 40–50 kati ya mimea kwa aina bora. Hata hivyo, baada ya mbegu kuota punguza idadi ya miche iliyopandwa huku ukiacha miche miwili tu ili kupata msongamano bora wa mimea. Panda mwanzoni mwa mvua ili kuwezesha mbegu kuota vizuri na kustawi.
Weka mbolea kwa wakati ufaao kutoka kwa washauri wanaoaminika ili kupata mavuno mengi.