Pilipili isipokaushwa vizuri hupata unyevu, na ukungu huota na kutoa sumukuvu amabayo ni hatari kwa watu. Kikaushaji cha jua hutumia joto la jua kukausha pilipili.
Kukaushia kwa jua kuna faida kadhaa: pilipili hukauka kwa muda mfupi, hubakia na rangi yake nyekundu, huzuia ukungu, haiwezi kuingiza uchafu na vile vile hukausha vyakula aina mbalimbali.
Kutengeneza kikaushaji cha jua.
Vifaa: Mbao, misumari, bawaba, kufuli na damani ya plastiki.
Anza kwa kutengeneza fremu ya mbao kutegemea ukubwa wa bati. Paka bati rangi nyeusi ili kuvuta kiasi kingi cha joto la jua. Kisha tengeneza kikaushiaji kilicho na kina cha 30 cm. Urefu wote uwe wa 95cm kwa mbele na 110cm kwa nyuma.
Kwa bati la urefu wa mita 3, tumia jozi 3 za miguu ili kisimame vizuri. Upande wa juu wa kisanduku unainuliwa kidogo. Tengeneza mbinu ya kusaidia kutelezesha trei ikiwa 10cm juu ya sakafu ya kikaushiaji. Kwa upande wa nyuma, tengeneza milango 2 ya kusaidia kuweka na kuondoa trei kwa urahisi. Funika fremu za trei kwa nyavu ili hewa iweze kufikia chakula kutoka pande zote mbili. Telezesha trei ndani, ikiwa 10cm kutoka kwenye sakafu ili kukausha hewa inapitia na kukausha pilipili vizuri. Mwishowe funika upande mrefu kwa chandarua ili kuzuia vumbi na wadudu kuingia. Weka kufuli ndogo ya kufungia mlango.
Mchakato wa kukaushia kwa jua
Osha mikono ili kudumisha usafi wa bidhaa. Weka kikaushiaji kwenye eneo lililo na jua. Tandaza pilipili safi kwenye trei halafu uziweke kwenye kikaushiaji. Hakikisha umefunga milango kila wakati ili nzi wasiingie. Ikiwa kuna baridi usiku, weka kikaushiaji ndani ya nyumba ili kudhibiti ukungu
Baada ya kuanika kwa siku 2 angalia ikiwa pilipili zimekauka, kisha uzifungashe na kuzihifadhi.